Dayaframu ya kuzuia mimba ni nini?
Dayaframu ni kijikombe chenye kina kifupi cha umbo wa kuba kilicho na mzingo laini inayonyumbulika, ambacho kinawekwa juu ya shingo ya kizazi kabla ya kufanya ngono. Kwa kawaida inaingizwa ndani kabisa mwa uke. Unapoingiza dayaframu ndani ya uke wako, inafunika shingo ya kizazi na kuweka manii nje ya mji wa mimba. Kabla ya kuiingiza ndani ya uke, lazima dayaframu ifunikwe na dawa ya kuua manii.
Ingawa dayaframu zinazopatikana kwa kawaida zimetengenezwa kwa ulimbo wa mpira (latex), dayaframu zilizotengenezwa kwa plastiki au silicone zinapatikana maeneo mengine.
Dayaframu zinapatikana kwa ukubwa mbalimbali na ili uweze kuzitumia vizuri, mara ya kwanza utahitaji kupimwa au upate maagizo maalum ya kujipima kutoka kwa mtoa huduma za matibabu aliyehitimu. Kuna uwezekano utapimwa fupanyonga ili kubaini ukubwa utakao kufaa (1).
Dayaframu ya kuzuia mimba hufanya aje kazi?
Dayaframu huzuia mimba kwa kuweka kizuizi halisi ambacho kinazuia manii kuingia kwenye shingo ya kizazi. Zaidi ya hayo, inashikilia dawa ya kuua manii kwenye shingo ya kizazi na kusitisha kusonga kwa manii yoyote itakayofika karibu na shingo ya kizazi. Tofauti na kofia ya shingo ya kizazi, ambacho kinashikiliwa kutokana na kufyonzwa, dayaframu inashikiliwa na ukuta wa uke (2).
Ufanisi wa dayaframu
Ufanisi wa dayaframu inategemea jinsi unavyoitumia.Ingawa ina ufanisi wa wastani, inafanya kazi bora zaidi ikitumiwa kwa kila tendo la ngono na ikiwa pamoja na dawa ya kuua manii.
Kwa matumizi ya kawaida (jinsi watu wengi wanavyoitumia) ina ufanisi wa asilimia 83 wa kuzuia mimba. Hii inamaanisha kuwa wanawake 17 kati ya 100 wanaoitumia watashika mimba ndani ya mwaka wa kwanza ya matumizi.
Kwa matumizi sahihi ( ikitumiwa pamoja na dawa ya kuua manii)ina ufanisi wa asilimia 84 wa kuzuia mimba,kumaanisha kwamba wanawake 16 kati ya 100 wanaotumia njia hii watashika mimba ndani ya mwaka wa kwanza ya matumizi (3).