Kondomu za ndani ni nini?
Kondomu za ndani,pia zinazojulikana kama kondomu za kike-ni vipochi au ala zinazoingizwa kwenye uke au mkundu kupata kinga dhidi ya mimba (wakati wa ngono ya ukeni) na magonjwa ya zinaa (STI). Zimeundwa kwa utando mwembamba angavu na zinatoshea kwenye uke kwa njia legevu.
Zina pete zilizolegea pande zote mbili. Pete kwenye sehemu imefungwa inatumiwa kuingiza kondomu ilhali pete kwenye sehemu iliyo wazi inatumiwa kushika kipande cha upande wa juu wa kondomu nje ya uke au mkundu.
Kondomu ya kike inaweza kutengenezwa kwa nyenzo mbalimbali kama vile nitrile, latex, au polyurethane.
Je, kondomu za ndani hufanyaje kazi?
Zinafanya kazi sawa na kondomu za nje, isipokuwa zinavaliwa ndani ya uke au mkundu badala ya uume. Zinaweka manii ndani ya kondomu na nje ya uke au mkundu. Pia zinasaidia kuzuia maambukizi au umajimaji ya kingono kwenye uume, uke au mkundu usifikie mwenzi (1)
Ufanisi wa kondomu za ndani
Ufanisi wa kondomu ya ndani unategemea jinsi unavyoitumia.Hatari ya mimba au kupata magonjwa ya zinaa inaongezeka ikiwa hautatumia kondomu kila mara unafanya ngono.Unaweza tu kushika mimba wakati unatumia kondomu ya kike kwa sababu ya matumizi yasiyo sahihi, kupasuka au kuteleza.
Inavyotumika kwa kawaida, watu 21 kati ya 100 wanaotumia kondomu ya ndani hushika mimba ndani ya mwaka wa kwanza ya matumizi. Hii inamaanisha kwamba ina ufanisi wa asilimia 79. Kwa matumizi kamilifu, ni wanawake 5 kati ya 100 wanaotumia kondomu ya ndani hushika mimba . Hii inamaanisha kwamba inaweza kuwa na ufanisi wa hadi asilimia 95 wa kuzuia mimba. Kondomu za ndani pia zinapunguza hatari ya kuambukizwa na magonjwa ya zinaa, ikiwemo VVU (2).