Ingawa ngono salama ni jukumu la wanaume na wanawake, mambo ya uzazi wa mpango imechukuliwa tangu kitambo kama jukumu la mwanamke. Ingekuwa wanaume wangechukua jukumu la kutumia njia za kuzuia mimba pia, visa vya mimba zisizopangwa na mangonjwa ya zinaa (STDs) vingepungua.
Katika makala hii, nitazungumzia umuhimu wa wanaume kujihusisha na mambo ya afya ya kizazi na pia njia bunifu yetu kuchukua jukumu la ngono salama, na haswa kuanza kuzungumzia swala hilo bila kuona haya. Ikiwa wewe ni mwanamume, kuwa makini; na ikiwa wewe ni mwanamke anayetaka mwenzi wake ahusike kwenye mchakato huu, mpatie makala hii asome na muanze mazungumzo.
1. Chukua uongozi kwa kuzungumzia uzazi wa mpango
Wanaume huchukulia ngono kuwa tu tendo la kuwapa furaha. Kwa ajili ya uelewa na elimu mdogo kuhusu ngono, tunachukulia kwamba kwavile hatuwezi kushika mimba, swala la uzazi wa mpango halituhusu na ni mambo ya wanawake. Lakini hili silo ukweli, kwasababu mimba isiyopangwa ikitokea, sote tutawajibika. Pia, magonjwa ya zinaa hayabagui wanawake kwa wanaume, sote tunahitaji kujikinga. Ndio maana wanaume wanastahili kuchukua uongozi wa kuzungumzia mambo ya uzazi wa mpango na wenzi wao. Hili litafanya wote wawili wafanye maamuzi bora.
Tunapozungumzia haya, ni muhimu kukumbuka kwamba swala la kijinsia linaathiriwa na imani ya kitamaduni na kidini. Kwa mfano, kwenye tamaduni zingine nchini Kenya, inachukuliwa kama ujeuri ukiomba ngono au ukiizungumzia moja kwa moja bila kutumia maneno yanayoonekana yenye heshima. Kwahivyo, ndoa inachukuliwa kama kupata ‘jiko’ na wakati msichana ana mimba kuna kabila zingine husema “miguu ya mbuzi yamevunjika”. Wakati tunazungumzia uzazi wa mpango, tuzingatie eneo mwenzi wetu anatoka na imani yake, na kulingana na haya au hisia zake, tunaweza taja maneno hayo moja kwa moja au tuyazungumzie kwa njia ya ucheshi.
2. Fanya utafiti na utambue njia na watoaji tofauti
Wanaume mara nyingi hawasaidi wenzi wao kuchagua njia ya uzuiaji mimba au watoa huduma kwasababu huwa hatuzungumzii swala hilo.
Tukichangia, tunaweza kufanya maamuzi bora zaidi na kupunguza uwezo wa kuchagua njia ambayo haifai.
Mazungumzo haya yanaweza kufanywa wakati wa kuzungumzia uzazi wa mpango. Mkifanya hivi pamoja, mnaweza kuboresha uhusiano wenu, na pia kuwapa fursa ya kuboresha ngono kati yenu.
Kulingana na aina ya uhusiano wetu, kuna chaguo mbalimbali tunazo:
- Njia za homoni za kubaki mwilini kwa muda mfupi, kama vile tembe za uzuiaji mimba;
- Njia za uzuiaji mimba za kuendelea kufanya kazi kwa muda mrefu kama vile IUD
- Njia ya kuzuia manii kwa wakati mmoja, kama vile kondomu; na
- Ufungaji uzazi, kama vile kufunga mirija ya uzazi (kwa wanawake) na vasektomi (kwa wanaume)
Wakati wa kutambua njia ya uzuiaji mimba sahihi, tunastahili kuzingatia imani ya kitamaduni na ya kidini ya mwenzi wetu. Kwa mfano, wakatoliki nchini Kenya, ambao ni asilimia 80 ya wakristo wote humo, wanaamini kwamba kutumia kondomu au njia za uzuiaji mimba ni kufanya dhambi. Ni vyema kuzungumzia haya na kukubaliana kutumia njia iliyo salama na inayokubaliwa na nyote wawili.
Kuna mambo mengine muhimu kuzingatia kabla ya kuchagua, wakati wa kuchagua na baada ya kuchagua njia ya uzuiaji mimba, kwa mfano, ufanisi wake, ikiwa inaweza kusitishwa ikishaingia mwilini, urahisi wa kuitumia, madhara yake na ikiwa inakubaliwa na nyinyi nyote. Na pia tunastahili kukuwa na mpango wa dharura au njia ya ziada ikiwa njia tunayotumia kwa kawaida itafeli, k.m. ikiwa kondomu itapasuka.
3. Hudhuria miadi na mwenzi wako na ulipie gharama ya njia za uzuiaji mimba
Njia za uzuaji mimba zina gharama! Unahitaji kuwekeza hela na wakati wako; na kama wanaume, tunastahili kuchangia kubeba gharama sawa na wanawake. Mbali na kuwa na jukumu la kutumia njia za uzuiaji mimba na kustahimili madhara zao, wanawake pia hubeba gharama ya kulipia njia hizi. Kama wanaume, tunaweza kusaidia kwa kuwasindikiza kwenda kwa mtoaji huduma na kuwapa msaada wa kihisia na kihela.
Wakati tukifanya hivi tunakuwa wenzi wa kutegemewa, pia inasaidia kukabiliana na fikira na ubaguzi wa kitamaduni, ambayo huwa na mtazamo mbaya kwa wanawake wanaonunua au wanaotumia njia za uzuiaji mimba. Mtazamo huu hutokana na unyanyapaa ulioko kwa swala la ngono ambalo hulifanya vigumu kwa watu, hata waliokomaa, kuzungumzia ngono na njia za uzuiaji mimba kwa uwazi. Imani hizi za kitamaduni huchukua ubikira kuwa jambo bora zaidi na ngono kuwa kitu kibaya. Hili linasababisha unyanyapaa katika uhisiano za mapenzi na ubaguzi wa kijinsia. Lugha inayotumika kuzungumzia mada hizi pia huwa ya siri. Kwamfano, lugha inayotumika mitaani nchini Kenya huita sehemu za siri “vitu.” Kuelewa ngono hivi huwafanya vijana kufanya ngono yao ya kwanza kwa usiri, uoga na kutokuwa na uhakika. Hali hii huweka afya yao ya kizazi kwenye hatari.
Kujishughulisha zaidi kwenye mambo ya uzazi wa mpango kwa kujielemisha, kuwa na mazungumzo wazi kuhusu kijinsia na mwenzi wetu, kuenda miadi na kutembelea watoaji huduma, kupanga kuhudhuria mikutano na kulipia gharama za njia za uzuiaji mimba, kunaweza kusaidia kurekebisha makosa.
4. Saidia kukabiliana na madhara
Tulivyosema hapo juu, njia za uzuiaji mimba zinaleta madhara; Ni madhara za kawaida lakini wakati mwingine zinaweza kuenda muda mrefu wakati mwanamke anapoanza kutumia njia mpya ya uzuiaji mimba. Kumsaidia mwenzi wetu wakati kama huu kunaweza kuwasaidia kuvumilia madhara hizi na ndio kwa maana ni muhimu kujua kuzihusu mapema. Wakati mwingine, hatujui jinsi ya kusaidia kwasababu hatuna uelewa; hili hufanyika ikiwa hatujajishughulisha toka mwanzo. Tukijishughulisha kutoka mwanzo, tutaweza kuzungumza kuhusu kupambana na madhara kwa urahisi.
Madhara moja ni kukuwa na mzio wa ulimbo wa mpira (latex) uliotumika kutengeneza kondomu- na kondomu ni njia inayotumika zaidi nchini Kenya. Ikiwa mwenzi wetu ana mzio wa latex, wanaweza kupata mwasho na pia kuwa na kamasi puani; tembe za kupunguza mzio; mafuta ya kupoesha mwasho kama vile calamine; au krimu ya kumaliza mwasho zinaweza kutumika. Njia ingine maarufu ya uzuiaji mimba ni tembe ya ‘morning after’ inayojulikana Kenya kama tembe ya dharura, P2 ama Femiplan. Madhara inayoleta ni kama kichefuchefu na ulaini wa matiti. Tunaweza kunywa chai ya tangawizi iliyo na mdalasini na pia kuoga maji moto kupunguza madhara.
Kila njia ya uzuiaji mimba huwa na madhara yake. Ukiwa unahusika kutoka mwanzo utapata habari na utapata uwezo wa kusaidia mwenzi wako kuvumilia.
5. Zingatia njia za uzuiaji mimba za wanaume
Njia nyingi za uzuiaji mimba ni za wanawake, na watu hawataki kujaribu za wanaume. Kwahivyo uzito uko kwa wanawake, hata ikiwa wana matatizo ya kiafya au ikiwa hawawezi kupata kwa urahisi njia za uzuiaji mimba.
Kujihusisha kwa mambo ya uzazi wa mpango na kutafuta chaguo pamoja itafanya iwe rahisi kwetu wanaume kuzizingatia. Kwa wakati huu, kuna tu aina mbili za njia za uzuiaji mimba kwa wanaume: Kondomu na vasektomi. Kuna utafiti unaendelea wa tembe za wanaume. Hili linaweza kuongezea pakubwa kwa chaguo za njia za uzuiaji mimba.
Kama mwenzi anayewajibika, tunapaswa kuchunguza mambo mazuri na mabaya kwa kila njia ya uzuiaji mimba. Na tuchague ile ni bora kwetu sote.
6. Mapambano kwa haki bora ya wanawake na chaguo zaidi kwa wanaume.
Haki za uzazi wa mpango na za kutoa mimba haziko ama kama ziko zinapuuzwa ndani ya nchi nyingi. Ni muhimu wanaume kupaza sauti kuzungumzia mambo haya ili kuwaunga mkono wanawake. Harakati za uzazi wa mpango zinapata umaarufu nchini Kenya. Hili linaokena kwa vyama kama Kenya SRHR Alliance, ambalo linaleta pamoja asasi za kiraia 17. Vikundi hivi vinatetea na kuhamasisha afya na haki ya kizazi ya vijana, wanawake na jamii zilizo tengwa.
Kujiunga na mapambano ni njia moja ya wanaume kupigania upatikanaji wa huduma za afya kwa wanawake na kutafuta njia bora na zaidi za uzuiaji mimba kwa wanaume. Tunaweza kufanya hivi kwa kutoa ufadhili kwa mashirika za mitaa au kwa kujiunga na maandamano na shughuli za kuhamasisha uelewa wakati zinaendelea. Tukiwa na sauti nyingi, itakuwa rahisi kwa waunda sera kutunga sera zitakazofaa.
Kampeni moja tunayoweza kujiunga nayo kwenye mtandao ni kuhusu huduma za afya ya kijinsia na kizazi (SHR) zilizo bora, zinazopatikana na zilizo bora kwa vijana. Kampeni ingine ni kuomba serikali ya mitaa kuongeza bajeti ya SHR. Hili ni kwa ajili ya kuboresha elimu ya maswala ya ngono na utafiti kwa njia za uzuiaji mimba kwa wanaume. Kampeni hizi zinaweza kuleta mabadiliko kwenye sera za serikali na kuhakikisha kwamba njia za uzuiaji mimba zinapatikana na ni za bei nafuu kwa kila mtu.
Wanaume wakichagua kuwajibika kwa swala la ngono, tutamaliza uoga na ukosefu wa uhakika. Na tutaweza kukuwa na maisha ya ngono kamili na wenzi wetu. Hatutaki tu hali ambayo wanaume wengi zaidi wanazungumzia haki bora ya afya ya kizazi. Tunataka wanaume wote waizungumzie.
Je, una jambo la kusema?Wacha ujumbe wako hapa chini, wasiliana nasi kwenye kurasa zetu za mitandao ya kijamii: Facebook, Instagram na Twitter au tutumie barua pepe kwenye info@findmymethod.org. Kwa taarifa zaidi kuhusu njia za uzuiaji mimba, tembelea findmymethod.org
Kuhusu mwandishi: Chris Mukasa ni mwandishi aliye Nairobi, Kenya. Yeye pia ni mwanzilishi wa Fatuma’s Voice, shirika la kijamii linalotumia sanaa, mashairi,majadiliano na muziki kuhamasisha vijana wazungumze bila uoga barani Africa.